Breaking

Jumatatu, 13 Oktoba 2025

TRA NA MAMLAKA YA MAPATO YA NORWAY WABADILISHANA UJUZI KATIKA USIMAMIZI WA WALIPA KODI WAKUBWA.

 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato ya Norway (NTA –The Norway Tax Revenue Authority) imeanza programu maalum ya kubadilishana ujuzi na uzoefu katika usimamizi wa kodi, hususan kwa Walipakodi Binafsi wa Hadhi ya Juu (High Net Worth Individuals – HNWIs). Mafunzo haya yanafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 13 hadi 17 Oktoba 2025.

Programu hii inalenga kuwajengea uwezo watumishi wa TRA katika kutambua, kuchambua na kusimamia kwa ufanisi masuala ya kodi yanayohusiana na walipakodi binafsi wenye hadhi ya juu. Pia inalenga kuboresha zaidi utoaji wa huduma bora kwa walipakodi wakubwa na kuimarisha mifumo ya kikodi kwa mujibu wa viwango na mbinu bora za kimataifa.

Kupitia ushirikiano huu, TRA na NTA wanabadilishana uzoefu wa kikazi na mbinu za kiutendaji zinazohusu usimamizi wa kodi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.

Mwenyeji wa programu ya mafunzo haya kutoka TRA ni Meneja wa Kodi za Kimataifa kutoka Idara ya Walipakodi Wakubwa, Ndugu Alfred Mkinga, ambaye ameeleza kuwa programu hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kikodi kati ya Tanzania na Norway, sambamba na kujenga uwezo endelevu wa ndani katika usimamizi wa kodi za walipakodi binafsi wa hadhi ya juu.

Programu hii inatarajiwa kuchangia kuongeza tija ya ukusanyaji wa mapato kwa Walipa kodi wakubwa. kukuza ufanisi wa kiutendaji ndani ya TRA, na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha mifumo ya kodi inabaki thabiti, shirikishi na yenye uwazi.

Hakuna maoni: