Serikali imekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa hatua kubwa ilizopiga katika mageuzi ya kidigitali, utafiti, maendeleo ya kitaaluma pamoja na mipango na mikakati ya kuboresha ufanisi wa utoaji wa mafunzo na ushauri wa kitaalam, hatua zinazotajwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025–2050.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula, alipomwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, wakati wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha yaliyofanyika mkoani Arusha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Luswetula amesema mchango wa IAA katika kukuza uchumi wa Taifa ni mkubwa, kwani chuo hicho kimeendelea kuzalisha wataalam mahiri katika nyanja mbalimbali zikiwemo fedha, uhasibu, uchumi, kodi, utalii, usimamizi wa biashara, benki, ununuzi na ugavi, masoko, bima pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Ameeleza kuwa wataalam hao wamekuwa mhimili muhimu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, usimamizi wa fedha za umma, kuimarisha sekta binafsi, taasisi za kifedha pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kupitia wahitimu wake, IAA imechangia kwa vitendo kukuza uwajibikaji, uwazi na nidhamu ya kifedha nchini.
Aidha, Serikali imekisifu Chuo cha IAA kwa kuwa kinara katika kuboresha mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia teknolojia za kisasa, sambamba na kuimarisha tafiti na utoaji wa ushauri wa kitaalam unaolenga kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli, amesema chuo hicho kimejipanga kuendelea kuzalisha wahitimu mahiri kwa kuwekeza zaidi katika rasilimali watu, hususan wahadhiri wenye sifa, uzoefu wa kitaaluma na kitaalam, pamoja na kuimarisha mbinu shirikishi za ufundishaji na ujifunzaji.
Naye Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema chuo kinaendelea kuimarisha huduma za ufundishaji na ujifunzaji ili kuendana na mabadiliko ya kasi ya mahitaji ya soko la ajira na uongozi wa kitaifa. Amefafanua kuwa hatua hizo zinahusisha maboresho ya mitaala, mbinu za ufundishaji pamoja na mifumo ya tathmini, kwa kuzingatia sera, mikakati na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025–2050.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni