Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Mkutano wa 11 wa Bahari Yetu “Eleventh Our Ocean Conference” (OOC11) uliofanyika Jijini Mombasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi nchini Kenya, ukihusisha viongozi wa Serikali, mashirika ya kimataifa, taasisi za utafiti, asasi za kiraia, sekta binafsi na wadau wa Bahari Duniani kote.
Mkutano huo ulitoa jukwaa muhimu la kujadili masuala ya usimamizi endelevu wa Bahari na uchumi wa buluu, ikiwemo uhifadhi wa bioanuwai za Baharini, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira ya Bahari, mifumo ya ikolojia ya Kaboni ya buluu, pamoja na maendeleo endelevu ya uchumi unaotegemea rasilimali za Bahari.
Katika mkutano huo, NEMC iliwakilisha Tanzania katika majadiliano ya ngazi ya juu na vikao vya kitaalamu vya pembezoni vilivyolenga kuimarisha mshikamano na mashirikiano ya kikanda na kimataifa katika kuhifadhi na kusimamia rasilimali za Bahari na maeneo ya pwani.
NEMC ilisisitiza dhamira ya Tanzania katika kuendeleza usimamizi shirikishi wa Bahari, uhifadhi wa mazingira, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya uchumi wa buluu unaozingatia uendelevu.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni