Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyowasilishwa katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, uteuzi huo ulianza rasmi Januari 19, 2023. Uteuzi huo unalenga kumshirikisha msanii huyo katika shughuli mbalimbali za kimataifa zinazohusu muziki, utamaduni na uwezeshaji wa wanawake.
Katika majukumu yake mapya, Witness anatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika mikutano na matukio ya kikanda na kimataifa, pamoja na kuhamasisha ushirikiano wa kiutamaduni kati ya nchi za Afrika. Pia atatumia nafasi hiyo kutangaza muziki na utamaduni wa Tanzania katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
Aidha, msanii huyo amealikwa kushiriki katika mkutano na tamasha la African Women in Music Summit & Concert – Second Edition, litakalofanyika nchini Afrika Kusini kuanzia Juni 21 hadi 28, 2026. Tukio hilo litawakutanisha wasanii, viongozi wa sekta ya utamaduni, watunga sera, watayarishaji wa muziki na wadau mbalimbali wa tasnia ya muziki kutoka mataifa tofauti barani Afrika.
Waandaaji wa mkutano huo wamesema lengo kuu ni kuimarisha ushirikiano, kukuza sauti za wanawake katika muziki wa Afrika na kuendeleza mtandao wa fursa ndani ya tasnia ya muziki duniani.
Katika nafasi yake kama balozi, Witness pia atasaidia kuimarisha mahusiano kati ya taasisi za Tanzania na wadau wa sekta ya ubunifu barani Afrika, huku akihamasisha usawa, uongozi na uwezeshaji wa wanawake kupitia muziki.
Taasisi ya 54 African Mamas ni jukwaa la Afrika linalolenga kuunganisha na kuinua sauti za wanawake kupitia muziki, ushirikiano wa kimataifa na diplomasia ya kitamaduni.
Witness Mwaijaga Sigbjorn amekubali uteuzi huo na kueleza kuwa yuko tayari kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na kwa manufaa ya Tanzania pamoja na maendeleo ya sekta ya muziki barani Afrika.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni