Breaking

Ijumaa, 15 Agosti 2025

BILLNAS NA NANDY WAPONGEZWA NA TRA KWA UZALENDO WA KODI

 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amewapongeza wasanii maarufu William Lyimo, almaarufu Billnas, na Faustina Mfinanga, almaarufu Nandy, kwa kujitokeza kulipa kodi kwa hiari. Ametoa pongezi hizo tarehe 14.08.2025 alipotembelewa na wasanii hao katika ofisi yake jijini Dar es Salaam.

Bw. Mwenda amewashukuru wasanii hao kwa kuonyesha mfano wa kuigwa katika kulipa kodi, na kusema kuwa hatua yao ni ishara ya uzalendo wa kweli unaochangia maendeleo ya taifa. 

“Ulipaji kodi wa hiari ni msingi wa kujenga uchumi imara, nawapongeza Billnas na Nandy kwa moyo wa kizalendo,” amesema Bw. Mwenda 

Kwa upande wake Bw. Billnas amesema, uzalendo wa kweli ni kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa. 

“Kodi tunayolipa inaleta mabadiliko chanya katika jamii, ikiwa ni pamoja na miundombinu bora na huduma za umma.” amesema Billnas

Kwa upande wake Bi. Nandy ameipongeza TRA kwa juhudi zake za kusimamia ukusanyaji wa kodi na kuelezea umuhimu wa kodi katika kuimarisha sekta mbalimbali. 

“Kodi inayokusanywa inasaidia kuinua tasnia ya muziki na sekta zingine nchini. Nawasihi wenzangu wasanii na Wananchi wote kulipa kodi kwa hiari ili tuijenge Tanzania bora,” amesema Nandy.

Wasanii hao wamejitolea kuwa mabalozi wa kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari, wakiahidi kushirikiana na TRA katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.



Hakuna maoni: