Wakazi wa Dodoma na Mikoa ya jirani wamefidika na elimu ya lishe bora inayotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete-JKCI katika maonesho ya 32 ya Kitaifa ya Nanenane.
Elimu hiyo imejikita kuwasaidia wananchi kubadili mtindo wa maisha utakaowasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya Moyo yanaoongoza kwa vifo vingi duniani.
Jijini Dodoma, Afisa Lishe kutoka JKCI, Emmanuel Lingindo, amesema huduma ya lishe ni sehemu muhimu ya matibabu kwa watu mwenye magonjwa ya moyo, watu wenye uzito mkubwa na watu wenye tatizo la shinikizo la damu.
Lingindo, amesema jamii pia inatakiwa kuacha matumizi ya sigara na unywaji wa pombe uliokithiri kwani kwa kutumia vilevi hivyo pia wapo katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Katika maonesho haya ya Nanenane hadi leo tumeweza kutoa elimu ya lishe bora kwa wananchi 70 ambapo kati yao wapo tuliowakuta na uzito mkubwa, shinikizo la damu na wengine wanaotumia vilevi kupindukia, kama watafuata ushauri wetu watakuwa salama”, amesema Lingindo.
Naye, mwananchi aliyetembelea banda la taasisi hiyo, Rehema Msemwa, amesema elimu aliyopata kuhusu lishe itamsaidia kupunguza uzito ili alinde moyo wake usipate madhara yanayoweza kusababishwa na uzito mkubwa na mafuta mengi mwilini.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni