Breaking

Alhamisi, 18 Septemba 2025

NEMC YAJA NA UKAGUZI MAALUM WA MAZINGIRA KATIKA MIRADI KWA MFUMO WA MTAA KWA MTAA

 Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linafanya ukaguzi maalum wa mazingira katika miradi mbalimbali nchini, ambapo ukaguzi huo unatekelezwa kwa mfumo wa mtaa kwa mtaa.


Ukaguzi huu unalenga kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira, sambamba na kuhakikisha miradi yote inazingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake.


Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa ya ukaguzi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria, Jamal Baruti, amesema Baraza linaendesha zoezi hilo kwa miradi ya maendeleo iliyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi cha wiki nne, kuanzia Septemba 15 hadi Oktoba 12, mwaka huu.


Baruti amesema lengo kuu la ukaguzi huo ni kuhakikisha kuwa miradi yote, yenye vyeti  na vyeti isiyo na vyeti, inakaguliwa na kuzingatia matakwa ya kisheria pamoja na kanuni zake. 


Aidha, ukaguzi wa awamu hii unafanyika kwa kutumia mfumo wa kidijitali ujulikanao kama Mazingira App, utakaohifadhi na kuratibu taarifa zote zitakazokusanywa.


Vilevile, Baruti ameongeza kuwa zoezi hili ni la nchi nzima na linatekelezwa kwa kushirikiana na ofisi za Serikali za mitaa. 

Amezitaka pia mamlaka nyingine na wadau mbalimbali kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hakuna maoni: