Breaking

Jumatano, 10 Septemba 2025

UCHUMI WA BULUU KUCHOCHEA MAENDELEO YA TAIFA

 Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Abdallah Mitawi, amesema kuwa Ofisi yake inaendelea kuratibu na kutekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo inalenga kuchochea uchumi wa Taifa na kuinua maisha ya Watanzania.

Mitawi ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wadau wa Uchumi wa Buluu 2025, linalofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili, likiwa na kauli mbiu: "Bahari Yetu, Fursa Yetu, Wajibu Wetu." Kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma, binafsi na kimataifa kujadili namna ya kunufaika na rasilimali zilizopo kwenye mazingira ya baharini na maji mengine.

Ameongeza kuwa mafanikio ya sekta hii yanahitaji mshikamano wa kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha uchumi wa buluu unakuwa chanzo kikuu cha pato la taifa.

Kwa upande wake, Profesa Tumaini Gurumo, Mkuu wa Chuo cha Bahari, amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kujadili maendeleo ya uchumi wa buluu sambamba na hali ya kiuchumi ya wananchi.

Aidha, Mwakilishi kutoka Wizara ya Uchukuzi, Mhandisi Shomary Shomary, alieleza kuwa Tanzania imefanikiwa kutumia njia za maji, zikiwemo Bahari ya Hindi na maziwa makuu matatu, kuimarisha uchumi wa buluu kwa kiwango kikubwa.

Kongamano hili linaweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kinara wa uchumi wa buluu duniani, kwa kuwa linahusisha taasisi mbalimbali ndani ya nchi na kushirikisha sekta za fedha na kimataifa, zenye dhamira ya kuimarisha uchumi wa bahari kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Hakuna maoni: