Shirika la Plan International limezindua kampeni ya #GirlsTakeover jijini Dar es Salaam leo, yenye lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia na kupambana na ndoa za utotoni. Uzinduzi huo umefanyika katika hoteli ya Four Points by Sheraton na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta za elimu, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Bi. Jane Sembuche, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, ambayo huadhimishwa kila tarehe 11 Oktoba duniani kote.
Kwa mujibu wa Plan International, ndoa za utotoni bado ni changamoto kubwa katika jamii nyingi, na zinachangia kukatisha ndoto na fursa za kielimu kwa wasichana. Kupitia hafla hii, shirika hilo limeweka msisitizo juu ya umuhimu wa serikali, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla kuungana kupinga vitendo hivyo na kuwekeza katika elimu na ustawi wa watoto wa kike.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Sheria kutoka TAWWA, Bi. Tike Mwambipele, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni, alisema wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuhakikisha wasichana wanapatiwa elimu bora, ulinzi na fursa za kushiriki katika uongozi.
Mmoja wa wasichana walioshiriki katika programu ya ‘Girls Takeover’, Unosye Atufigwege, alisema elimu aliyopata kupitia mpango huo imempa ujasiri na kuonyesha kwamba mtoto wa kike anaweza kuwa kiongozi bora endapo ataandaliwa vyema na kulindwa dhidi ya vikwazo kama ndoa za utotoni.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba, yakilenga kuhamasisha uwezeshaji wa watoto wa kike na kulinda haki zao katika jamii.
#Official-Isharoja✍🏾



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni