Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda zimekubaliana kuongeza wigo wa ushirikiano wa kimkakati katika sekta muhimu za kiuchumi kwa lengo la kukuza uchumi wa mataifa hayo jirani na rafiki ya Afrika Mashariki pamoja na ustawi wa watu wake.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Februari 7, 2026, katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kati ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mgeni wake Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliyekuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Rais Dkt. Samia akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuhitimisha mazungumzo hayo, mbali na kuelezea mafanikio yaliyofikiwa katika ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), amebainisha kuwa wamekubaliana kuendelea kufanya kazi kwa pamoja sambamba na kuongeza ushirikiano katika sekta muhimu za kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wake, Rais Museveni amekumbusha na kusisitiza umuhimu wa pande zote mbili, na Afrika kwa ujumla, kusimamia maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi, ikiwa ni mojawapo ya njia za kuenzi malengo ya uhuru wa Afrika na kutimiza maono ya waasisi wake.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni