Breaking


Jumamosi, 7 Februari 2026

SHAYKAA APEWA HADHI YA KIMATAIFA: BALOZI WA BODI YA FILAMU TANZANIA NCHINI INDIA




Bodi ya Filamu Tanzania imemtambua rasmi mwanatasnia mashuhuri wa filamu, Bi. Shahista Alidina maarufu kama Shaykaa, kuwa Balozi wa Bodi ya Filamu Tanzania katika sekta ya filamu nchini India, hatua inayotarajiwa kuipa tasnia ya filamu ya Tanzania fursa mpya kimataifa.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, alimkabidhi Shaykaa cheti maalum cha kuthibitisha ubalozi wake katika hafla iliyofanyika Ijumaa, Februari 6, 2026, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kukuza na kuitangaza filamu ya Tanzania nje ya nchi.

Shaykaa ni mtayarishaji na msanii wa filamu wa Tanzania anayeheshimika kimataifa. Mwaka 2021, aliipeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya kushinda Tuzo ya World Oscars Signature ya Mwigizaji Bora wa Kike kupitia uigizaji wake katika filamu Uhuru na Gharama Zake. Ushindi huo uliiweka filamu ya Tanzania katika ramani ya majukwaa makubwa ya kimataifa.

Kwa miaka kadhaa sasa, Shaykaa amekuwa daraja muhimu kati ya wadau wa filamu wa Tanzania na masoko ya kimataifa, hususan nchini India, mojawapo ya masoko makubwa ya filamu duniani.

Kupitia nafasi yake mpya ya ubalozi, Shaykaa anatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kibiashara kati ya tasnia za filamu za Tanzania na India, kuitangaza Tanzania kama kituo bora cha kurekodia filamu, pamoja na kufungua fursa za ubia, mafunzo na usambazaji wa filamu za Kitanzania katika soko la dunia.

Hatua hii inaonesha dhamira ya Bodi ya Filamu Tanzania katika kutumia wasanii wenye uzoefu wa kimataifa kuisukuma mbele tasnia ya filamu na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha ubunifu wa filamu barani Afrika na duniani. 🎬🌍

Hakuna maoni: