Breaking


Jumamosi, 2 Mei 2026

TRA YAKAMATA TANI 27 ZA MAGENDO YA MACADAMIA TARAKEA, KILIMANJARO

 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kukamata tani 27 za zao la macadamia zilizokuwa zikiingizwa nchini kinyume cha sheria kupitia mpaka wa Tarakea, wilayani Rombo.

Operesheni hiyo ilifanyika usiku wa kuamkia Aprili 29, 2026, ikiwa ni sehemu ya doria za kawaida zinazofanywa na maofisa wa forodha wa TRA katika kudhibiti biashara haramu mipakani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shehena ya macadamia ilikamatwa ikiwa tayari imepakiwa kwenye magari mawili aina ya Fuso, yakisubiri kuingizwa nchini bila kufuata taratibu za kisheria.

Maofisa wa forodha walifanikiwa kunasa mzigo huo baada ya ufuatiliaji makini, hatua inayoonesha kuimarika kwa udhibiti wa mipaka dhidi ya vitendo vya magendo.

Kwa sasa, magari hayo pamoja na mzigo vimehifadhiwa chini ya usimamizi wa Idara ya Forodha ya TRA, huku uchunguzi ukiendelea na hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi ya wahusika wa tukio hilo.

TRA imeendelea kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuzingatia sheria na taratibu za biashara halali, ikisisitiza kuwa vitendo vya magendo vinaathiri uchumi wa nchi na mapato ya serikali.


Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa udhibiti wa magendo ni muhimu katika kulinda soko la ndani, kuongeza mapato ya serikali na kuhakikisha ushindani wa haki kwa wafanyabiashara wanaofuata sheria.


Hakuna maoni: