Breaking


Jumamosi, 2 Mei 2026

TRA TANGA YAKAMATA MADUMU 148 YA MAFUTA YA MAGENDO


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Tanga imefanikiwa kukamata madumu 148 ya mafuta ya kupikia yaliyokuwa yakisafirishwa kinyume cha sheria, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti magendo nchini.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Aprili 30, 2026 katika eneo la Mwakidila, Wilaya ya Tanga, ambapo maafisa wa Kitengo cha Kudhibiti Magendo walifanya operesheni maalum na kufanikiwa kuyakamata mafuta hayo. Bidhaa hizo zilikuwa zinasafirishwa kwa kutumia gari aina ya Toyota Hiace.

Kwa mujibu wa Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, kukamatwa kwa bidhaa hizo ni matokeo ya kuimarishwa kwa doria na operesheni dhidi ya wafanyabiashara wanaokiuka sheria za kodi na uingizaji wa bidhaa nchini.

Amesisitiza kuwa magendo yana athari kubwa kwa uchumi wa taifa, ikiwemo kupotea kwa mapato ya serikali ambayo hutumika kugharamia huduma za kijamii kama afya, elimu na miundombinu.

Mbali na hilo, alionya kuwa bidhaa za magendo mara nyingi huwa hazijathibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hali inayoweza kuhatarisha afya na usalama wa watumiaji.

TRA imeendelea kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kufuata taratibu sahihi za uingizaji wa bidhaa nchini pamoja na kulipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Hatua hizi zina lengo la kulinda uchumi wa nchi, kuhakikisha ushindani wa haki kwa wafanyabiashara halali, na kulinda afya ya watumiaji.


Hakuna maoni: