Breaking


Jumapili, 3 Mei 2026

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

Serikali imeeleza dhamira yake ya kuimarisha uzalishaji wa maziwa nchini kwa kuendeleza miradi ya ufugaji wa kisasa, huku Shamba la Mifugo la Kitulo mkoani Njombe likitajwa kuwa moja ya maeneo muhimu yatakayosaidia kufikia lengo hilo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bashiru Ally Kakurwa, amesema kuwa mahitaji ya maziwa nchini yameendelea kuongezeka, hali inayolazimu kuchukuliwa kwa hatua madhubuti za kuongeza uzalishaji kupitia upatikanaji wa mitamba bora ya ng’ombe wa maziwa.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Shamba la Mifugo la Kitulo Mei 2, 2026, Waziri huyo alisema kuwa licha ya mwamko unaoendelea kwa wafugaji kuingia katika ufugaji wa kisasa, bado kuna upungufu wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa ukilinganisha na mahitaji yaliyopo.

Alifafanua kuwa ongezeko la mahitaji ya maziwa nchini linatoa fursa kubwa ya kiuchumi kwa wafugaji, lakini pia linaweka wazi umuhimu wa kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa mifugo bora.

“Wananchi wamehamasika kufuga kisasa. Ingawa si wote, lakini idadi inaongezeka. Hata hivyo, mahitaji ya maziwa ni makubwa kuliko uzalishaji, hivyo ni muhimu kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa hapa nchini,” alisema Waziri Kakurwa.

Aidha, Waziri huyo alimuagiza Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kuhakikisha kuwa kupitia mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, shamba hilo linapatiwa takribani ng’ombe 3,000 wa maziwa ili kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya mifugo, Fabian Madele, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wataalamu na wadau wa sekta ya mifugo ili kufanikisha malengo ya serikali ya kuboresha rasilimali za mifugo nchini.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Rabson Mahenge, alisema halmashauri hiyo imekuwa ikishirikiana na uongozi wa shamba hilo kulinda eneo dhidi ya uvamizi, hatua inayolenga kuhakikisha linaendelea kutumika kikamilifu kwa uzalishaji wa mifugo bora.

Uwezo wa Shamba la Kitulo

Shamba la Mifugo la Kitulo lina ukubwa wa takribani hekta 4,875.641. Kwa sasa lina uwezo wa kuhifadhi ng’ombe 1,500, huku likiwa na uwezo wa kupanuliwa na kufikia hadi ng’ombe 4,500 kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa na nyama.

Uwekezaji katika mashamba ya mifugo kama Kitulo ni hatua muhimu katika kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa uzalishaji wa maziwa, kupunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi, na kuongeza kipato kwa wafugaji kupitia ufugaji wa kisasa.

Hakuna maoni: