Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto ya makazi kwa vijana, ambapo Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema vijana walioanza ajira hivi karibuni pamoja na wale waliojiajiri watapewa kipaumbele katika upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa nyumba 144 za gharama nafuu zilizojengwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, Ulega alisema mpango huo unalenga kupunguza mzigo wa gharama za makazi kwa vijana, hasa katika maeneo ya mijini yenye msongamano mkubwa wa watu.
Alieleza kuwa serikali imechukua hatua hiyo baada ya kutambua changamoto kubwa inayowakabili vijana katika kupata makazi bora na nafuu, hali inayochangia kupungua kwa ufanisi kazini kutokana na muda mwingi kupotea kwenye safari za kila siku.
“Kwa mujibu wa takwimu za sensa, bado kuna upungufu mkubwa wa nyumba nchini. Hivyo, serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi kushughulikia changamoto hii kwa vitendo,” alisema Ulega.
Aliongeza kuwa mbali na Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameidhinisha ujenzi wa miradi kama hiyo katika mkoa wa Dodoma na miji mingine mikubwa nchini ili kuongeza upatikanaji wa makazi nafuu.
Kwa mujibu wa maelezo ya mradi huo, kati ya nyumba 144 zinazojengwa, nyumba 72 ni za chumba kimoja, sebule, jiko na choo, huku nyingine 72 zikiwa na vyumba viwili, kimoja kikiwa ni self-contained pamoja na sebule, jiko na choo cha pamoja.
Ulega alibainisha kuwa vijana wengi hulazimika kuishi mbali na maeneo yao ya kazi kutokana na uhaba wa nyumba za gharama nafuu mijini, hali inayosababisha matumizi makubwa ya muda na fedha katika usafiri.
Alisisitiza kuwa ujenzi wa nyumba hizo katika maeneo ya mijini yenye fursa nyingi ni mkakati wa serikali wa kuongeza tija kwa vijana kwa kuwawezesha kutumia muda mwingi zaidi katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, alieleza kuwa mpango wa nyumba za gharama nafuu ni sehemu ya mikakati ya muda mrefu ya maendeleo ya taifa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu, ikiwemo makazi bora.
Serikali imeahidi kuendelea kupanua miradi hiyo katika mikoa mbalimbali kulingana na mahitaji, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha usawa wa upatikanaji wa makazi kwa wananchi wote, hususan vijana.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni