Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewapokea na Viongozi na Wataalamu wa hali ya hewa kutoka Taasisi ya Hali ya Hewa ya Burundi (IGEBU) na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Sudan Kusini (SSMS) kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kuhusu Utabiri wa Hali ya Hewa kwa Njia za Mahesabu (NWP), utabiri wa hali mbaya ya hewa, na mifumo ya usimamizi wa ubora (QMS). Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili 2026 Tanzania.
Mafunzo haya yameandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kupitia Mradi wa Kuboresha Mfumo wa Utoaji wa Tahadhari za Hali Mbaya ya Hewa (CREWS). Mafunzo yanalenga kuwajengea uwezo wa utaalamu na mbinu bora katika utoaji wa huduma za hali ya hewa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akifungua programu ya mafunzo hayo kwa vitendo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, alisisitiza dhamira ya Tanzania kupitia TMA katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika masuala ya huduma za hali ya hewa.
“Mafunzo haya yanaonesha dhamira yetu thabiti ya kuboresha huduma za hali ya hewa si tu nchini Tanzania bali katika ukanda mzima wa Afrika. Kupitia ushirikiano na mafunzo haya, tunaweza kuboresha utoaji wa huduma na kujenga uimara na ustaimilivu dhidi ya changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Tunafuraha kubwa kuwakaribisha hapa TMA katika Ofisi zetu za Dodoma na Dar es Salaam.”Alizungumza Dkt. Chang'a.
Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Bw. Zablon Shilenje alitoa shukrani kwaniaba ya Mkurugenzia wa WMO Afrika, Dkt.Agnes Kijazi kwa uongozi wa Tanzania na dhamira yake katika kutoa ushirikiano wa kikanda.
“Tunashukuru Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano hususani katika eneo la kuwajengea uwezo wataalamu wa hali ya hewa kutoka Afrika ikiwemo Sudan Kusini na Burundi. Ni muhimu tusonge mbele pamoja na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika uboreshaji huduma za hali ya hewa".Alisema Bw. Zablon
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa IGEBU, Bw. Deogratias Babonwanayo, alipongeza mpango huo:“Tunashukuru kwa fursa ya kushirikiana na TMA na kujifunza kutokana na uzoefu wao katika utekelezaji wa mifumo ya usimamizi wa ubora. Mafunzo haya yatachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma zetu nchini Burundi.”
Kwa upande wake, Bw. Mojwok Ogawi Modo, Mkurugenzi Mkuu SSMS, alieleza umuhimu wa ziara hiyo:“Ziara hii itatoa nyenzo muhimu kwa vitendo na kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu na washirika wa kikanda hususani Tanzania. Tunaamini kwamba mafunzo tunayoyapata hapa yatachangia kuboresha huduma za hali ya hewa nchini Sudan Kusini".
Ziara hii ya vitendo inaakisi uwekezaji endelevu wa Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya hali ya hewa, na kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni