Breaking


Jumatano, 15 Aprili 2026

MASAUNI: BARAZA LA WAFANYAKAZI NI NGUZO YA UFANISI NA UWAJIBIKAJI SERIKALINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema mikutano ya Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la kujadili utekelezaji wa majukumu, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na weledi. 

Amehimiza umuhimu wa kudumisha utamaduni wa kufanya kazi kwa umoja, bidii na taaluma ili kuongeza ufanisi na tija katika utendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais.

Akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika Dodoma Aprili 15, 2026, Masauni amesema Ofisi hiyo imeendelea kufanya vizuri katika kudumisha Muungano pamoja na kutoa elimu kwa umma kwa makundi mbalimbali. 

Pia ameainisha mafanikio katika usimamizi wa mazingira, ikiwemo marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Sura 191) na kuanzishwa kwa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Amesisitiza haja ya kuimarisha uwezo wa kitaalam na kitaasisi, kuongeza upatikanaji wa rasilimali na kuhamasisha fedha kupitia maandalizi bora ya miradi ya uhifadhi wa mazingira. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema baraza hilo limekuwa chombo muhimu cha kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango, pamoja na kuboresha uhusiano kati ya menejimenti na watumishi. 

Alibainisha kuwa mkutano huo unalenga kuwasilisha na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya Ofisi. 

Hakuna maoni: