Breaking


Alhamisi, 28 Agosti 2025

𝐖𝐀𝐓𝐔𝐍𝐙𝐀𝐊𝐔𝐌𝐁𝐔𝐊𝐔𝐌𝐁𝐔 𝐖𝐀 𝐓𝐅𝐒 𝐖𝐀𝐏𝐀𝐓𝐀 𝐓𝐔𝐙𝐎 𝐊𝐖𝐄𝐍𝐘𝐄 𝐌𝐊𝐔𝐓𝐀𝐍𝐎 𝐌𝐊𝐔𝐔 𝐖𝐀 𝐓𝐑𝐀𝐌𝐏𝐀


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeibuka kinara katika Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Watunzakumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) baada ya watunzakumbukumbu wake kutunukiwa tuzo mbili na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa.

Tuzo hizo ni ya ufadhili wa mkutano na ya taasisi yenye washiriki wengi zaidi. Waziri Mkuu Majaliwa alizikabidhi jana Agosti 27, 2025 kwa Josephine Solomon, Askari wa Uhifadhi Mwandamizi wa TFS, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulianza Agosti 25 na unatarajiwa kuhitimishwa Agosti 28, 2025, ukiwakutanisha watunzakumbukumbu na wataalamu wa nyaraka kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Ushindi huo umeelezwa kuwa ni matokeo ya uongozi wa TFS kuruhusu ushiriki mpana wa watunzakumbukumbu kutoka makao makuu, kanda na mashamba, hatua iliyoiwezesha taasisi hiyo kupewa tuzo ya washiriki wengi zaidi.

Aidha, menejimenti ya TFS ikiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, imeshukuriwa kwa kutambua nafasi ya watunzakumbukumbu katika kuboresha utendaji wa taasisi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu Majaliwa alizitaka taasisi zote kuhakikisha mifumo ya usimamizi wa kumbukumbu na taarifa inaimarishwa na inasomana ili kurahisisha utendaji na uwajibikaji.

Alielekeza pia:

Waajiri wasimamie utekelezaji na kuripoti hatua zilizofikiwa;

Watunzakumbukumbu walinde siri za Serikali na kuzingatia maadili ya kazi;

Wakaguzi washirikiane na wataalamu wa kumbukumbu wakati wa ukaguzi;

Taarifa ziweze kupatikana kwa wakati inapohitajika;

Watunzakumbukumbu wapewe stahiki zao, nafasi za mafunzo na motisha kazini;

Taasisi zichangie ujenzi wa Kituo cha Maarifa cha TRAMPA kitakachojengwa Dodoma.


Mkutano wa mwaka huu unalenga kuboresha taaluma ya usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka nchini, sambamba na mageuzi ya kidijitali na kukuza ufanisi katika utumishi wa umma.

Hakuna maoni: