Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuanza rasmi zoezi la ukaguzi wa mita za umeme kwa wateja wake kote nchini. Hatua hii inalenga kudhibiti upotevu wa mapato na kubaini wateja wasio waaminifu wanaotumia umeme bila kulipia.
Tangazo hilo limetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Huduma kwa Wateja ya Kinondoni Kusini iliyopo Kibamba. Uzinduzi huo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo kuboresha huduma na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
“Tumekuwa na changamoto ya upotevu wa mapato kutokana na mita zilizozeeka na kushindwa kufanya kazi vizuri, lakini pia kutokana na baadhi ya wateja wasio waaminifu wanaochezea mita kuiba umeme. Zoezi hili litahakikisha tunazikagua mita hizo na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaobainika,” alisema Bi. Gowelle.MFUMO WA TAARIFA ZA SIRI
Bi. Gowelle amewataka wananchi kutumia mfumo wa utoaji taarifa za siri uliyozinduliwa hivi karibuni ili kufichua wahujumu wa rasilimali za shirika hilo. Amewahakikishia watoa taarifa hao usalama na ulinzi wa hali ya juu.
OFISI MPYA KIBAMBA
Katika hatua nyingine, Bi. Gowelle amepongeza uongozi na wafanyakazi wa Kinondoni Kusini kwa kufanikisha ujenzi wa ofisi mpya, akisema hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza muda wa kushughulikia changamoto za wateja.
Amesisitiza pia matumizi sahihi ya umeme kama nishati salama na rafiki wa mazingira, akihamasisha wananchi kuunga mkono kampeni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kupikia kwa gharama nafuu.
WITO KWA WAFAKAZI
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Kibamba, Bi. Salma Yahya Muharam, amemshukuru mgeni rasmi kwa kushiriki katika uzinduzi huo na ameipongeza Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa ofisi hiyo. Ameitaka timu yake kuendelea kushirikiana ili kupunguza malalamiko ya wateja na kutoa huduma bora zaidi.
HATUA KALI KWA WEZI WA UMEME
TANESCO tayari limeanza kuwakamata na kuwachukulia hatua baadhi ya wateja wanaoiba umeme au kujiunganishia kinyume cha sheria katika maeneo mbalimbali nchini. Shirika hilo limesema litaendeleza ukaguzi huu kwa wigo mpana zaidi ili kuhakikisha huduma bora na uendelevu wa sekta ya umeme nchini.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni