Breaking

Jumanne, 23 Septemba 2025

OUSMANE DEMBÉLÉ ATAWAZWA MSHINDI WA BALLON D’OR 2025

Winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Ousmane Dembélé, ameibuka kidedea kwa kutwaa Tuzo ya Ballon d’Or 2025 baada ya kumzidi chipukizi wa Barcelona, Lamine Yamal, ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa kutokana na ubora aliouonyesha msimu uliopita.


Dembélé (28), ambaye kwa kawaida hucheza pembeni mwa uwanja kama winga, aling’ara kwa kiwango cha juu msimu huu akiwa sehemu muhimu ya kikosi cha PSG kilichotwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa kihistoria wa mabao 5–0 dhidi ya Inter Milan. Mbali na mafanikio hayo, pia aliisaidia klabu yake kutwaa ubingwa wa Ligue 1, akionyesha kuwa ni mchezaji muhimu wa mashambulizi na mchangiaji mkubwa wa mabao.


Kwa mujibu wa takwimu za msimu wa 2024/25, Dembélé alicheza jumla ya mechi 53, akifunga mabao 35 na kutoa assist 16, huku akicheza kwa jumla ya dakika 3,488 katika mashindano yote. Hii ndiyo rekodi iliyomfanya aonekane bora zaidi kuliko washindani wake, na hatimaye kushinda tuzo kubwa zaidi ya soka duniani.


Mashabiki wa PSG wameeleza furaha yao kupitia mitandao ya kijamii wakimtaja Dembélé kama “mkombozi wa kweli” wa klabu hiyo, huku wachambuzi wakikiri kwamba 2024/25 ilikuwa msimu bora zaidi katika maisha yake ya soka.


Kwa ushindi huu, Dembélé amejiunga rasmi na orodha ya wachezaji wachache waliowahi kushinda Ballon d’Or, na kuimarisha nafasi yake kama mmoja wa winga bora duniani kwa sasa.


#BallonDor2025

#OusmaneDembele

#PSG

#UEFAChampionsLeague

#Ligue1

#FootballNews

#MadelemoNews

#SokaUlaya

#LamineYamal

#WachezajiBora


Hakuna maoni: