Serikali imetangaza kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vituo vyote vya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) nchini, ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na nafuu kwenye vyombo vya moto.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo kipya cha Puma Energy kilichopo Bagamoyo Road jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa gesi kwa wananchi.
“Serikali inafanya jitihada hizi ili kutoa nafasi kwa Watanzania kutumia gesi kwenye vyombo vyao vya moto, kwa kurahisisha upatikanaji wake na kwa kuwa matumizi ya gesi yana gharama nafuu zaidi ikilinganishwa na mafuta,” amesema Mhandisi Mramba.
Aidha, Serikali imeondoa kodi kwenye vifaa vya kufunga mifumo ya gesi katika magari na bajaji, hatua inayotarajiwa kuongeza uhamasishaji wa matumizi ya gesi asilia.
Kwa sasa, jijini Dar es Salaam kuna vituo 11 vya kujazia gesi kwenye magari, huku Serikali ikidhamiria kufikisha vituo 18 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Vilevile, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeshaingiza magari sita maalumu yatakayozunguka maeneo mbalimbali kutoa huduma ya kujaza gesi.
Mhandisi Mramba aliipongeza Puma Energy kwa uwekezaji huo na kuwataka wadau wengine kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya CNG.
“Natoa wito kwa wananchi na watumiaji wa vyombo vya moto kuendelea kutumia gesi asilia, kwani vituo vimeongezeka na huduma sasa ipo karibu zaidi na jamii,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy, Bi. Fatma Abdallah, alisema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa kampuni kuunga mkono jitihada za Serikali katika mageuzi ya matumizi ya nishati safi na salama kwa vyombo vya moto.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni