Mwanariadha nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu, amewasili nchini alfajiri ya leo kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, akitokea Tokyo, Japan, alikoshinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika yaliyofanyika Septemba 15, 2025.
Mapokezi ya Simbu yalikuwa ya aina yake, yakiongozwa na Maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), familia yake, mashabiki, viongozi wa michezo, wanariadha wenzake, na wananchi waliojitokeza kwa wingi kumpokea shujaa huyo wa taifa.
Katika mashindano hayo ya dunia, Simbu alikimbia kwa kasi ya kuvutia na kumaliza mbio hizo ambapo alionesha ujasiri na nguvu ya ziada katika sekunde za mwisho kwa kumpita Amanal Petros wa Ujerumani.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Simbu alisema ushindi huo ni wa Watanzania wote huku akiimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika Sekta ya Michezo hususan kwa kutoa hamasa mbalimbali kwa wanamichezo ambazo zinawasaidia katika kujituma.
Aidha amesmhukuru Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob Mkunda kwa kuendelea kuamini nafasi ya Michezo na kutoa nafasi kubwa katika michezo Jeshini.
Serikali imetangaza hafla maalum ya kumpongeza Simbu itakayofanyika Septemba 27, 2025, jijini Dodoma, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atamkabidhi zawadi maalum kwa kulitangaza taifa kimataifa kupitia michezo.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni