Breaking

Jumatano, 15 Oktoba 2025

KATIBU MKUU AFYA AHIMIZA KUFANYA MAZOEZI KULINDA AFYA

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, ametoa wito kwa watumishi wa umma  wakiwemo wale wa  wizara anayoiongoza ya Afya na Watanzania kwa ujumla kuzingatia afya zao wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa kufanya mazoezi, kula mlo sahihi na kupata muda wa kupumzika.

Dkt. Shekalaghe ametoa wito huo mapema  Oktoba 14, 2025, Jijini Dar es Salaam, wakati akizindua kitabu kiitwacho  “From Muscle to Brain” kilicho andikwa na Dkt. Catherine Kahabuka.

“Kitabu hiki mafunzo yake muhimu  ni kuwakumbusha watumishi kuzijali afya zao kwa kuhakikisha wanapata muda wa kupumzika na familia zao, kufanya mazoezi, na  kujiepusha na msongo wa mawazo ili kuwa na afya njema ya akili na mwili,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Aidha Dkt. Shekalaghe  amewataka wataalam wa afya kutumia elimu yao kwa manufaa ya jamii kwa kutoa elimu kuhusu magonjwa mbalimbali  hususani magonjwa sugu yasiyoambukiza  ili kusaidia jamii kujikinga na kuyadhibiti.

Dkt. Shekalaghe pia alisema jamii inapata funzo  kupitia kitabu hicho kuhusu umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii hivyo  wataalam wa afya wasikae na maarifa bila kuyafikisha kwa wananchi hasa elimu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.

Pia kiongozi huyo amewahimiza madaktari na wauguzi kutumia taaluma zao kujiajiri badala ya kutegemea ajira za Serikali pekee, akibainisha kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wataalam hao kuanzisha hospitali, kliniki na maabara binafsi, hatua itakayoongeza ajira kwa vijana wengine.

Kwa upande wake Dkt. Catherine Kahabuka, ambaye ni mtunzi wa kitabu hicho,  amesema lengo la kitabu cha From Muscle to Brain ni kuwahamasisha watumishi wa umma na sekta binafsi kutumia taaluma na ubunifu wao kuunda fursa nje ya ajira rasmi, badala ya kutegemea ajira pekee.

Hakuna maoni: