Breaking

Jumapili, 30 Novemba 2025

EACLC LETENI WAFANYABIASHARA WENYE TEKNOLOJIA NA UJUZI AMBAO HAUPO NCHINI -KATAMBI

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi amekiasa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kufanya kazi na Wafanyabiashara Wageni wanaoleta teknolojia na ujuzi ambao haupo nchini ili kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanajifunza na kukuza biashara zao.

Katambi ameyasema hayo  Novemba 29, 2025, alipotembelea na kufungua Maonesho ya Kwanza ya Biashara ya EACLC, Ubungo jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa jukumu kuu la kituo hicho ni kuelimisha, kutangaza na kukuza biashara ndani na nje ya nchi.

Vilevile, Katambi amewasisitiza  wafanyabiashara nchini kutumia kikamilifu Maonesho hayo  katika kuongeza ubunifu, kupanua masoko na kuimarisha ubora wa bidhaa za Kitanzania.

Katambi pia amebaibisha umuhimu wa wafanyabiashara kuunganisha nguvu na kutumia majukwaa ya maonesho kama fursa ya kuongeza tija na ushindani katika soko la kikanda na kimataifa.

Aidha, Katambi ameipongeza EACLC Limited kwa kuandaa maonesho hayo muhimu ambayo yamewakutanisha washiriki zaidi ya 200 na watembeleaji wanaotarajiwa kufikia 1,000, akisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika Afrika Mashariki, Kusini na Kati.

Ametaka Washirika wa maonesho kutumia siku za maonesho kujenga mitandao mipya ya kibiashara, kuingia mikataba yenye tija na kuboresha bidhaa ili ziweze kushindana kimataifa, akisisitiza kuwa maendeleo ya viwanda hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EACLC Limited, Cathy Wang, amesema maonesho hayo yameandaliwa ili kuimarisha miundombinu ya biashara ikiwemo maghala, ofisi, maeneo ya maonyesho na huduma za usafirishaji, sambamba na kuwaunganisha wafanyabiashara na wateja wao moja kwa moja ili kuongeza uelewa wa bidhaa na fursa za uwekezaji.

Hakuna maoni: