Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, TMA, imetoa utabiri wa hali mbaya ya hewa kwa baadhi ya maeneo nchini kwa siku tano zijazo kuanzia tarehe 19 hadi 22 mwezi Novemba 2025. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, siku ya Jumatano hakutakuwa na tahadhari yoyote, hata hivyo angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa maeneo machache ya mikoa ya Ruvuma na Njombe, ambapo kiwango cha athari kinatarajiwa kuwa cha wastani.
Siku ya Alhamisi, mvua kubwa zinatarajiwa kuendelea katika maeneo kadhaa zaidi ikijumuisha mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Njombe, Morogoro, Singida, Dodoma, Kigoma, Katavi na Tabora. TMA inasema uwezekano wa mvua hizo kutokea ni wa kiwango cha wastani na zinaweza kusababisha athari ikiwamo baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, hivyo wananchi wanashauriwa kuchukua tahadhari.
Aidha, Ijumaa mvua kubwa zinatarajiwa kuendelea katika maeneo ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma, Morogoro, Singida na Dodoma, ambapo athari zinazoweza kujitokeza ni zilezile za makazi kuzungukwa na maji. Mamlaka hiyo imewataka wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia tahadhari zote muhimu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni