Dirisha dogo la usajili la Januari linakaribia kufunguliwa, na tayari tetesi zimeanza kutikisa ulimwengu wa soka, hususan kuhusu mustakabali wa mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mohamed Salah. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya michezo, inaelezwa kuwa klabu kadhaa kutoka Saudi Arabia zinajiandaa kufanya jitihada kubwa kumshawishi mchezaji huyo kujiunga na ligi yao.
Ligi ya Saudi Arabia imekuwa ikivutia wachezaji wakubwa duniani kwa muda sasa, na inaonekana mpango wao wa kuendelea kuimarisha ushindani hautarudi nyuma. Inaripotiwa kuwa ofa ambayo inaweza kuwasilishwa kwa Liverpool Januari huenda ikawa ya kiwango cha juu mno maarufu kama “life-changing offer” na huenda ikawatia moyo viongozi wa Liverpool kuketi mezani kusikiliza.
Kwa upande wa Liverpool, bado hakuna taarifa rasmi kuhusu kama watakuwa tayari kumruhusu mchezaji wao muhimu kuondoka katikati ya msimu, ikizingatiwa umuhimu wa Salah ndani ya kikosi cha kocha Jürgen Klopp. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa soka wanadai kuwa kama ofa itakuwa kubwa kiasi cha kuifanya klabu kutafakari upya mipango yao, basi huenda Januari ukawa mwezi wa maamuzi magumu.
Kwa sasa, mashabiki wa Liverpool wanasubiria kwa hamu kuona kitakachojiri, huku wakiendelea kumkubali Salah kama nguzo muhimu ya mafanikio ya timu hiyo. Je, dirisha la Januari litaleta mabadiliko makubwa? Je, Saudi Arabia itaongeza nguvu katika mbio za kumsajili mfalme huyo wa Anfield?
Tunasubiri tuone jinsi tetesi hizi zitakavyoendelea kujichanua kadri siku zinavyosogea.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni