Breaking


Ijumaa, 8 Agosti 2025

NAIBU WAZIRI KIPANGA: TUHIFADHI MAZINGIRA KWA KUPANDA NA KUTUNZA MITI

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga, leo ametembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya NaneNane yanayoendelea jijini Dodoma na kutoa pongezi kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi kubwa ya uzalishaji na uhifadhi wa miche bora ya miti.

Mhe. Kipanga alitembelea Kituo cha Uzalishaji wa Mbegu na Miche ya Miti Bora cha TFS kilichoko ndani ya banda hilo, ambako alishuhudia aina mbalimbali za miche inayozalishwa kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuinua uchumi wa wananchi.

“Leo tarehe nane Agosti, 2025, nimepata fursa ya kutembelea banda letu la Wizara ya Maliasili na Utalii na kwa kipekee idara yetu ya TFS ambayo inajihusisha moja kwa moja na uhifadhi wa rasilimali za miti nchini. Nimefurahishwa sana na kazi wanayofanya, kuanzia uzalishaji wa miche, utunzaji wa misitu hadi uhifadhi wa mapori ya asili,” alisema Mhe. Kipanga.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alipata nafasi ya kununua miche ya miti ya matunda kwa ajili ya kupanda kwenye eneo lake la makazi jijini Dodoma, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha mazingira na kujihakikishia upatikanaji wa matunda na kivuli katika siku za usoni.

“Miche hii itakapokuwa, itaniletea manufaa makubwa sana – kwa upande wa chakula, kivuli na hata kurejesha uoto wa asili. Hii ni sehemu ya juhudi zetu binafsi kama Watanzania katika kuhifadhi mazingira yetu,” aliongeza.

Akizungumzia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, Mhe. Kipanga alieleza kuwa tatizo hilo linasababishwa kwa kiwango kikubwa na ukataji holela wa miti na uharibifu wa misitu. Alisisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na kuitunza ipasavyo.

“Kupanda peke yake haitoshi. Tunapaswa kuhakikisha miti tunayopanda inatunzwa hadi kukua. Hii ni silaha muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa mvua unaolikumba taifa letu,” alisema.

Aidha, alitoa rai kwa wananchi na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kwenye mabanda ya TFS yaliyopo katika viwanja vyote vya Nanenane nchini ili kujifunza zaidi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo ya serikali.

Mabanda ya TFS yanapatikana katika viwanja vya Nanenane kwenye kanda zote.

Hakuna maoni: