Jukwaa la Ufugaji Nyuki Tanzania (TABEDO), likiwa ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya NaneNane 2025, limeendeleza kampeni yake ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa, maarifa na teknolojia ya kisasa ya ufugaji nyuki.
Kupitia ushirikiano na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), TABEDO imejipambanua kuwa kitovu cha maarifa, bidhaa na huduma zinazohusu nyuki kwa ajili ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Tunatumia jukwaa hili kuhamasisha ufugaji nyuki wa kisasa, kuonesha bidhaa kama asali, nta na virutubisho vinavyotokana na nyuki, lakini pia kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiunga na jukwaa letu,” amesema Katibu wa TABEDO, Bi. Catherine Peter.
Amesema mfumo wa usajili wa kidijitali ulioanzishwa na TABEDO unalenga kuwafikia watanzania wengi zaidi, hata wale ambao hawakuweza kufika katika viwanja vya maonesho. Kwa kutumia tovuti ya jukwaa hilo, wananchi wanaweza kujisajili kwa urahisi kwa ada ya Sh 7,175 pekee.
Tovuti hiyo ni: www.tabedo.or.tz
Bi. Peter amesema kuwa mfumo huo umebuniwa kwa kuzingatia urahisi wa matumizi na upatikanaji wa taarifa sahihi, huku ukiimarisha usimamizi na mawasiliano baina ya wanachama na viongozi wa TABEDO katika ngazi zote.
“Kwa wale wanaohitaji msaada zaidi, wanashauriwa kuwasiliana na viongozi wa TABEDO katika mikoa yao au kupitia mawasiliano ya moja kwa moja na ofisi ya jukwaa,” aliongeza.
Kwa mujibu wa TABEDO, sekta ya nyuki inatoa mchango mkubwa katika hifadhi ya mazingira, uzalishaji wa mazao kwa njia ya uchavushaji, na kuinua uchumi wa kaya hususan kwa vijana na wanawake wanaojihusisha na ujasiriamali wa bidhaa za nyuki.
Aidha, jukwaa hilo limebainisha kuwa jitihada za pamoja baina ya wadau wote ikiwemo taasisi za serikali, vyuo vya elimu ya mazingira, wafanyabiashara na mashirika ya kiraia zinaweza kuleta mapinduzi makubwa katika kukuza sekta ya nyuki kwa tija zaidi.
“Tunahitaji kushirikiana katika kuijenga sekta hii. Nyuki si tu chanzo cha asali, bali ni mhimili muhimu wa maisha ya binadamu na uendelevu wa mazingira,” amesema Bi. Peter.
Wananchi wote wanaopenda kupata maelezo zaidi kuhusu usajili au kushiriki shughuli za jukwaa hilo wanahimizwa kuwasiliana kupitia:
📞 0753 023 622
📧 tabedotz@gmail.com

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni