Leo, dunia inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanaotumia Mkono wa Kushoto, maarufu kama International Left-Handers Day. Siku hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Agosti tangu ilipoanzishwa mwaka 1976 na Dean R. Campbell wa Left-Handers International. Lengo kuu ni kuenzi, kutambua, na kuelimisha jamii kuhusu uzoefu wa watu wanaotumia mkono wa kushoto katika dunia iliyotengenezwa zaidi kwa wanaotumia mkono wa kulia.
Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa kati ya asilimia saba hadi kumi ya watu duniani ni left-handed. Wataalamu wanasema mara nyingi watu wa mkono wa kushoto huonyesha ubunifu wa hali ya juu na kufanikisha taaluma mbalimbali kama sanaa, muziki, michezo, na sayansi ya ubunifu. Hata hivyo, wanakabiliwa na changamoto kama vile uhaba wa vifaa maalum, meza na zana zilizoundwa kwa ajili ya mkono wa kushoto, na mitazamo potofu kutoka kwa jamii.
Shirika la Left-Handers International na taasisi nyingine zimeandaa matukio maalum ikiwemo mashindano, maonyesho ya vipaji, na warsha za kuhamasisha jamii. Wanahimiza shule, sehemu za kazi, na wazalishaji wa vifaa kuhakikisha vinakuwa rafiki kwa wote bila kujali mkono wanaotumia.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni