Breaking


Jumapili, 10 Agosti 2025

TRA YASISITIZA KODI KWA BIASHARA ZA MTANDAONI

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesisitiza kutekeleza agizo lake la kutoza kodi kwa biashara za mtandaoni, hususan huduma za malazi (online accommodation), ifikapo Septemba Mosi,mwaka huu 2025

Akizungumza  jijini Dar es Salaam  wakati wa uzinduzi wa kampeni ya elimu ya kodi kwa biashara za mtandaoni, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema licha ya muda wa usajili kuhitimishwa Agosti 31, baadhi ya wadau wamelalamika muda huo kutotosha na kuomba uongezwe.

Hata hivyo, TRA itatekeleza agizo hilo kama lilivyoelekezwa, kufuatia mabadiliko ya kifungu cha 51 cha Sheria ya Kodi, kitakachoanza rasmi Septemba 1 mwaka huu, kwa wamiliki wa mali za majengo yanayotoa huduma za malazi wanaotumia majukwaa ya mtandao.

Masharti hayo hayatahusu wafanyabiashara wadogo wanaotumia mitandao kwa kujitangaza, kwani wameongezewa muda.

Mwenda amesema TRA imeongeza muda kwa wafanyabiashara wadogo wanaotumia mtandao kujitangaza, ili kuwapa nafasi ya kupata elimu ya kutosha, kushiriki semina na kusajiliwa, ambapo mchakato wote utafanyika kwa njia ya mtandao.

Aidha, Mwenda amesema TRA imejipanga kutumia teknolojia kuwatambua wafanyabiashara wote wa mtandaoni na itahamasisha wanunuzi kutoa taarifa kwa mamlaka pale ambapo hawapati risiti, ambapo taarifa sahihi zitazawadiwa asilimia tatu ya kodi itakayokusanywa.

Hakuna maoni: