Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaendelea kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Mama Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, ambapo shughuli zinatarajiwa kufikia kilele chake kesho, 28 Septemba 2025.
Katika maonesho hayo, TFS inatumia fursa kuelimisha na kushirikisha wananchi kuhusu majukumu yake, yakiwemo uhifadhi wa misitu, upandaji miti, ufugaji nyuki, udhibiti wa moto, utalii ikolojia pamoja na fursa za uwekezaji katika misitu ya asili. Aidha, wananchi wanapewa elimu kuhusu faida za mazao ya nyuki ikiwemo asali, chavua, nta na bidhaa zinazotokana na misitu.
Akizungumza na wanahabari katika banda la TFS, Mhifadhi Juma Mdoe kutoka Shamba la Miti Silayo alisema taasisi hiyo inazalisha mazao bora ya nyuki na kuwataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi kushiriki katika shughuli za ufugaji nyuki badala ya kuendeleza ukataji miti holela.
“Tunawahamasisha wananchi na wadau kuwekeza katika ufugaji nyuki kwa kuwa ni shughuli endelevu inayoongeza kipato bila kuharibu mazingira. Pia kuna fursa za utalii na michezo ya kimazingira kama mbio za nyika katika Shamba la Miti Silayo na Rubare,” alisema Mdoe.
TFS, kupitia vitengo vyake ikiwemo Kituo cha Mbegu za Miti Morogoro na mashamba ya miti kama Silayo, inabaki mstari wa mbele katika kutoa elimu na kuhamasisha matumizi bora ya rasilimali misitu nchini.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni