Breaking

Jumanne, 30 Septemba 2025

TISEZA YAJA NA FURSA KUVUTIA WAWEKEZAJI KONGANI YA KWALA

 

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania TISEZA, imekuja na mikakati mipya ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kukuza ushindani na maendeleo ya sekta ya uwekezaji nchini.

Kupitia kongani ya kibiashara ya Kwala, iliyopo Kibaha mkoani Pwani, TISEZA inatoa fursa mbalimbali kwa wawekezaji, ikiwemo utoaji wa maeneo bure kwa wawekezaji watakaokamilisha ujenzi wa miradi yao ndani ya kipindi cha miezi 12.

Kaimu Ofisa Mawasiliano wa Umma wa TISEZA, Adelina Rushekia, ameeleza hayo wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika eneo la Kwala, Septemba 30, 2025. 

Amesema kongani hiyo yenye ukubwa wa hekta 100 ni miongoni mwa miradi inayotangazwa kwa sasa na mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa Adelina, wawekezaji wa ndani wanaruhusiwa kuwekeza kwa mtaji wa kuanzia Dola za Kimarekani milioni 5 sawa na takriban shilingi bilioni 12.5, huku wawekezaji wa nje wakitakiwa kuwa na mtaji wa kuanzia Dola milioni 10 sawa na shilingi bilioni 25.

Ametaja maeneo mengine yanayotangazwa na TISEZA kwa ajili ya uwekezaji ni Buzwagi mahsusi kwa ajili ya uchenjuaji wa madini na Nala, Dodoma.

Adelina anasema tayari wawekezaji 10 ambao wengi wao ni wazawa wameonyesha nia ya kuwekeza katika kongani ya Kwala.

Kwa upande wake, Gerald Tiria, msimamizi wa kiwanda cha kuzalisha majokofu kilichopo katika kongani hiyo, ameeleza kiwanda hicho kimeajiri vijana 30 wa Kitanzania, ambapo 25 kati yao wana mikataba ya ajira rasmi.



Mwamvua Mwinyi,Pwani.

Hakuna maoni: