Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda amani na tunu za taifa, akisisitiza kuwa misingi hiyo imeiwezesha Tanzania kudumisha utulivu kwa kipindi chote cha kabla na baada ya Uhuru.
Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini, wazee na wadau wa maendeleo jijini Dar es Salaam, viongozi wa dini walisema vijana wa kizazi cha sasa wanapaswa kuendeleza misingi ya uzalendo, maadili na mshikamano iliyoasisiwa na wazee waliolitumikia taifa katika hatua muhimu za historia yake.
Viongozi hao waliipongeza Serikali kwa kuimarisha huduma mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa barabara, kuboresha sekta ya afya na kusimamia ukuaji wa uchumi, hatua ambazo zimeongeza fursa kwa wananchi na kuchochea maendeleo katika maeneo mengi ya nchi.
Aidha, walisisitiza jukumu la taasisi za dini katika kuwaunganisha wananchi, kuhimiza utulivu na kufundisha maadili mema, wakisema kwamba mchango wao ni muhimu katika kuendeleza mshikamano unaolitambulisha taifa la Tanzania.
Akitoa msisitizo huo, DC Mpogolo alisema amani inahitaji ulinzi wa pamoja na kuwataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini mienendo inayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi. “Amani yetu ni tunu ya thamani. Naomba wananchi na viongozi wa dini msisite kutoa taarifa mtakapoona jambo lisilo la kawaida. Bila taarifa, hakuna hatua inayoweza kuchukuliwa. Tushirikiane kuilinda nchi yetu,” alisema Mpogolo.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni