Marufuku! Hilo ndilo neno linaloongoza hatua mpya iliyochukuliwa na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ambao leo Jumatano, Desemba 10, 2025, umetangaza kusitishwa kwa matumizi ya miundombinu ya mwendokasi kwa vyombo vyote vya moto isipokuwa mabasi maalum ya mfumo huo.
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha DART, imeelezwa kuwa vibali vyote vilivyowahi kutolewa awali vimesitishwa rasmi, na kwamba doria na udhibiti vitaimarishwa kuhakikisha agizo hilo linazingatiwa. Aidha, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maelekezo hayo.
Marufuku hii imekuja wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la magari ya Serikali na bodaboda kutumia barabara hizo maalum kinyume cha taratibu.
Novemba 25, 2025, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega aliwahi kuruhusu magari ya abiria kutumia barabara ya mwendokasi ya awamu ya tatu kwa muda, kutoka katikati ya jiji kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi Gongo la Mboto, ili kupunguza msongamano katika Barabara ya Nyerere. Ruhusa hiyo ilitolewa baada ya kukamilika kwa mradi huo kwa asilimia 100, ikisubiri mtoa huduma wa mabasi maalum kupatikana.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni