Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, ametekeleza ahadi yake ya kutoa cherehani za umeme kwa vikundi viwili vya akinamama wa Kata ya Kazimzumbwi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Kisarawe, inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia viwanda vidogo na vya kati.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi cherehani hizo, Dkt. Jafo amesema kuwa wakati wa kampeni aliahidi kuwawezesha akinamama wanaojishughulisha na viwanda vidogo, hususan shughuli za ushonaji, na leo ametimiza ahadi hiyo kwa kukabidhi cherehani vinavyotumia umeme kwa vikundi hivyo viwili vya akinamama.
“Leo nimepata fursa ya kutoa cherehani za umeme kwa vikundi vya akinamama; kikundi cha Darajani na kikundi cha Sanze vya Kata ya Kazimzumbwi ” amesema Dkt. Jafo.
Ameeleza kuwa ana imani kubwa kuwa cherehani hizo zitatumika ipasavyo katika kujenga uchumi wa akinamama hao na jamii kwa ujumla, ikiwemo kushona sare za wanafunzi, nguo za sherehe na mavazi mengine.
Aidha, amesema hatua hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutumia na kuendeleza viwanda vidogo vilivyopo katika maeneo yao kama njia ya kukuza uchumi wa ndani.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kazimzumbwi,Siza Juma Dilunga, amemshukuru Mbunge Dkt. Jafo kwa kutekeleza ahadi yake kwa akinamama hao, akisema uwezeshaji huo utawasaidia kujikwamua kiuchumi. Ameahidi kuwasimamia wanufaika hao ili kuhakikisha cherehani zilizotolewa zinatumika kwa tija na kuleta manufaa chanya kwa jamii.
Naye, Afisa Miradi kutoka Shirika la Sustainable Planet Foundation, ndugu Aloyce Kamando, amesema shirika hilo limekabidhi cherehani hizo za kisasa kupitia Ofisi ya Mbunge wa Kisarawe kwa lengo la kuchochea maendeleo ya wananchi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni