Serikali iko katika Maandalizi ya Usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka 18 ili kutoa namba ya utambulisho ya kipekee ambayo itatolewa tangu mtu anapozaliwa hadi mwisho wa maisha yake ikiwa ni Utekelezaji wa Maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyotoa tarehe 10 Agosti,2023.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene wakati wa ziara ya ukaguzi wa uzalishaji wa vitambulisho katika Kituo cha Kuchakata Taarifa cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) ambapo amaetaja kiasi cha Shilingi Bilioni 11.3 kutengwa kwa ajili ya zoezi huku wilaya za majaribio zikiwa ni Kilolo, Kusini Unguja na Rungwe ambapo pia ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kufika sehemu walizojiandikisha kuchukua vitambulisho vyao.
‘Jamii namba itakayotambua watoto ndio jambo kubwa ambalo linakuja sasa na itaondoa malalamiko mbalimbali kwani mtu atakua anatambulika kuanzia pale anapozaliwa lakini pia nawasihi watanzania ama ni walowezi ama wakimbizi na wengine wakawa wameombea kazi utambulisho sio wao au walisomea majina sio yao wakaondolewa kazini umetolewa msamaha na Mheshimiwa Rais kwamba waje wasafishe taarifa zao za utambuzi ili warudi kwenye majina yao yanayotambulika kwa kuwa hayo waliyokua wameyatumia yataendelea kuwaletea matatizo wakati wote,wengine wameondolewa kazini kwa vyeti feki na wengine wameshindwa kupata uraia kwa kuwa walitoa taarifa ambazo sio sahihi na wengine waliomba vitambulisho zaidi ya mara moja.’ Amesema Waziri Simbachawene
Simbachawene ameongeza pia kuna vitambulisho ambavyo vimezalishwa na wahusika hawajafika kuchukua akiwataka kufika vituo mbalimbali katika wilaya walizojiandikishia ili kuchukua vitambulisho vyao huku akiweka wazi ukomo wa matumizi ya namba ya utambulisho(NIN) kuwa ni miaka mitatu.
‘Watu wafike katika maeneo waliyojiandikisha kuchukua vitambulisho vyao kwani kitambulisho cha NIDA hivi sasa kimeunganishwa na Kadi ya Bima ya Afya,leseni ya udereva na mifuko ya hifadhi ya jamii hatua ambayo imemrahisishia mwananchi pindi anapotaka kupata huduma za kiafya au mfuko wa jamii.’ Aliongeza Waziri Simbachawene.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlala ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),Omar Mmanga amesema mamlaka inaendelea na utambuzi na usajili wa watanzania wanaoishi nje ya nchi(diaspora) ambapo jumla ya watanzania 1465 wanaoishi nje ya nchi wametambuliwa na kuandikishwa mpaka sasa huku lengo ikiwa kuwafikia watanzania wote wawe na utambulisho popote walipo ambapo mpaka sasa jumla ya vitambulisho 21,245,975 vikiwa vimezalishwa nchini.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni