Breaking

Ijumaa, 19 Desemba 2025

MAJIKO BANIFU YA RUZUKU YAPIGA HODI KATAVI


Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kununua majiko banifu kwa bei ruzuku ya shilingi 7,500 yanayosambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini-REA ili kulinda afya, kuokoa misitu na kuhifadhi mazingira.

Ametoa rai hiyo Mkoani Katavi wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza majiko banifu ya ruzuku yapatayo 3,126 unaotekelezwa na Kampuni ya Tango Energy Ltd ya Jijini Dar es Salaam.

Unaratibiwa na kusimamiwa na REA wenye thamani ya shilingi Milioni-156.3 ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia mwaka 2024-2034.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Katavi, amemshukuru Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo amejielekeza katika kuhakikisha kwamba wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia.

Akitambulisha mradi, Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka REA, Dokta Joseph Sambali, amesema majiko hayo yatauzwa kwa shilingi 7,500 badala ya shilingi elfu-59 kwa kuwa Serikali kupitia REA imetoa ruzuku ya asilimia 85 sambamba na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani-VAT katika majiko hayo ili kumpa unafuu mwananchi.

“Kabla ya ruzuku jiko moja lilikuwa likiuzwa kwa shilingi 59,000 na baada ya Serikali kuweka ruzuku likauzwa kwa shilingi 8,850 lakini sasa baada pia ya kuondoa kodi ya VAT jiko moja hapa Katavi litauzwa kwa shilingi 7,500 pekee," alibainisha Dkt. Sambali.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tango Energy Ltd, Musa Msofe, amesema wamejipanga ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwamba majiko hayo yatauzwa kwa bei ya ruzuku kwa mwananchi mwenye kitambulisho cha Taifa-NIDA na kwamba majiko hayo yana udhamini wa mwaka mmoja.

Hakuna maoni: