Breaking


Jumapili, 22 Februari 2026

DKT. ABBASI AFUNGA RASMI TFS SPORTS BONANZA 2026, KASKAZINI NA KANDA YA KATI WATWAA UBINGWA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amehitimisha rasmi Bonanza la Michezo la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS Sports Bonanza) leo Februari 22, 2026, baada ya siku tano za ushindani mkali, nidhamu na mshikamano miongoni mwa watumishi.

Bonanza hilo lililofanyika kuanzia Februari 18 hadi 22, 2026, liliwakutanisha kanda mbalimbali zikichuana katika mpira wa miguu, netiboli na michezo ya jadi ikiwemo bao, karata, darts na drafti, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha afya, umoja na ari ya utendaji kazi ndani ya taasisi.

Katika matokeo ya netiboli, Mashariki ilitwaa nafasi ya tatu kwa kuibuka na ushindi wa mabao 26–24 dhidi ya Magharibi. Fainali ya netiboli ilishuhudia Kanda ya Kati ikiibuka bingwa baada ya kuichapa SAO HILL kwa mabao 34–12, huku SAO HILL ikimaliza kama mshindi wa pili.



Kwa upande wa mpira wa miguu, Kanda ya Ziwa ilitwaa nafasi ya tatu kwa ushindi wa mabao 3–0 dhidi ya Nyanda za Juu. Katika mchezo wa fainali, Kaskazini iliibuka bingwa baada ya kuifunga SAO HILL mabao 2–0, huku SAO HILL ikiridhika na nafasi ya pili.


Mashindano hayo yalihitimishwa kwa shamrashamra na utoaji wa zawadi kwa washindi, yakionesha dhamira ya TFS kuendeleza michezo kama nyenzo ya kujenga timu imara na yenye mshikamano kazini.

Hakuna maoni: