Hakuna shaka kwamba Tetsuya Yamagami, mwanaume aliyemuua aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, mwaka 2022, atapatikana na hatia pindi mahakama itakapotoa uamuzi wake. Yamagami alikiri kosa hilo mapema mwanzoni mwa kesi iliyoanza mwaka jana, hatua iliyofunga mjadala kuhusu hatima ya kesi hiyo upande wa hatia.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 45 anatarajiwa kuhukumiwa leo, lakini adhabu anayostahili imeendelea kuzua mjadala mpana na maoni kinzani miongoni mwa wananchi wa Japan. Wakati sehemu kubwa ya umma inamchukulia Yamagami kama muuaji katili aliyefanya kosa lisilosameheka, wengine wanaonesha huruma, wakirejea maisha yake ya utotoni yaliyojaa misukosuko na mateso ya kifamilia.
Waendesha mashtaka wadai kifungo cha maisha
Upande wa mashtaka umeiomba mahakama imhukumu kifungo cha maisha gerezani, wakieleza kuwa kitendo cha kumpiga risasi na kumuua Shinzo Abe ni “uhalifu mzito” uliotikisa misingi ya usalama na utulivu wa taifa. Abe alikuwa kiongozi mashuhuri sana nchini Japan, taifa ambalo uhalifu wa kutumia bunduki ni nadra kupita kiasi, hali iliyofanya mauaji yake kuwa tukio la kushangaza na la kuumiza kwa jamii nzima.
Utetezi wasisitiza “unyanyasaji wa kidini”
Kwa upande wao, mawakili wa utetezi wanaiomba mahakama imuonee huruma Yamagami, wakidai kuwa alikuwa mhanga wa unyanyasaji wa kidini. Wanadai kuwa mama yake alijihusisha kwa kiwango kikubwa na Kanisa la Unification, hali iliyosababisha familia kufilisika kifedha.
Kwa mujibu wa utetezi, Yamagami alianza kumchukia Abe baada ya kugundua kile alichodhani kuwa ni uhusiano wa karibu kati ya waziri mkuu huyo wa zamani na kanisa hilo lenye utata.
Uchunguzi mpana wa Kanisa la Unification
Kifo cha kushtua cha Abe, aliyepigwa risasi mchana kweupe alipokuwa akihutubia hadhara, kilisababisha uchunguzi mpana kuhusu Kanisa la Unification. Uchunguzi huo ulifichua madai ya kukusanya michango mikubwa ya fedha kutoka kwa waumini wake, kiasi cha kuwaacha wengine wakiwa wameangamia kifedha.
Zaidi ya hayo, kesi hiyo ilifichua pia uhusiano wa karibu kati ya kanisa hilo na baadhi ya wanasiasa wa Chama cha Liberal Democratic Party (LDP) kinachotawala Japan, hali iliyosababisha mawaziri kadhaa kujiuzulu kufuatia shinikizo la umma.
Mauaji yaliyotikisa dunia
Shinzo Abe, aliyekuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Japan, alikuwa mmoja wa watu mashuhuri zaidi nchini humo wakati wa kifo chake. Mauaji yake hayakuishia kuishtua Japan pekee, bali yalitikisa dunia nzima, yakizua maswali kuhusu usalama wa viongozi wa kisiasa hata katika mataifa yanayojulikana kwa amani na nidhamu kali ya sheria.
Ombi la mwisho la utetezi
Katika hoja yao ya mwisho, mawakili wa Yamagami wameiomba mahakama imhukumu kifungo kisichozidi miaka 20 gerezani, wakisisitiza kuwa mteja wao alichukua hatua hizo kutokana na chuki aliyojengewa na mazingira ya kifamilia. Mahakama iliambiwa kuwa Yamagami alilichukia kanisa hilo baada ya mama yake kutoa kwa kanisa bima ya maisha ya marehemu baba yake pamoja na mali nyingine, zenye thamani ya takribani yen milioni 100.
Sasa macho na masikio ya dunia yako kwa mahakama ya Japan, huku wengi wakisubiri kuona uamuzi utakaochukuliwa katika kesi ambayo imeacha alama isiyofutika katika historia ya kisiasa na kijamii ya taifa hilo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni