Breaking


Alhamisi, 22 Januari 2026

MKURUGENZI MKUU NSSF AONGOZA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII SOKO LA TEGETA NYUKI


 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba, amesema hakuna sababu kwa mwananchi aliyejiajiri kushindwa kujiunga na Mfuko huo kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa ambayo yanawawezesha kunufaika na mafao mbalimbali sawa na waajiriwa wa sekta ya umma na binafsi.

Ametoa kauli hiyo wakati akiwaongoza  wafanyakazi wa NSSF kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kuandikisha wanachama wapya katika soko la Tegeta Nyuki jijini Dar es Salaam, kupitia kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi.

Amesema mwananchi atakayejiajiri na kujiunga na NSSF atanufaika na mafao ya pensheni ya uzeeni, urithi, ulemavu, uzazi, matibabu pamoja na mafao mengine ambayo awali hayakuwa yakipatikana kwa kundi hilo.

Mshomba ameeleza NSSF imeboresha mfumo wa uchangiaji kwa kuufanya kuwa rahisi na rafiki kwa wananchi, ambapo mwananchi anayechangia sh. 30,000 kwa mwezi atanufaika na mafao yote ikiwemo matibabu, huku anayechangia sh. 52,200 kwa mwezi atanufaika yeye, mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, Lulu Mengele, amesema kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi itaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.


Katibu wa soko hilo, Omary Hemed amewashukuru NSSF kwa kuendelea kufikisha elimu sokoni hapo na kuwapa fursa wajasiriamali mali kujiunga na kuchangia ambapo wengi wananufaika na mafao yanayotolewa yakiwemo ya matibabu.

Hakuna maoni: