Breaking


Ijumaa, 1 Mei 2026

WATUMISHI WA TUME YA MADINI WASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI KITAIFA NJOMBE


Watumishi wa Tume ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Lunyanywi, Halmashauri ya Mji wa Njombe.


Maadhimisho hayo yameongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na kuhudhuriwa na wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali nchini. Lengo kuu limekuwa ni kuenzi mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa, pamoja na kujadili ustawi wao na kuboresha mazingira ya kazi.


Katika tukio hilo, watumishi wa Tume ya Madini walishiriki maandamano rasmi sambamba na taasisi nyingine za umma na binafsi, wakionesha mshikamano wa wafanyakazi wa sekta ya madini. Ushiriki huo unaakisi dhamira ya sekta hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi kupitia rasilimali madini.

Kauli mbiu ya mwaka huu isemayo, “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” imelenga kuhamasisha ajira zenye heshima, kulinda haki za wafanyakazi, na kuimarisha mchango wao katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya nchi.


Kwa ujumla, maadhimisho ya Mei Mosi hufanyika kila mwaka duniani kote kama jukwaa muhimu la kutambua mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Pia ni fursa ya kuhimiza uboreshaji wa mazingira ya kazi ili kuhakikisha usalama, ustawi, na tija kwa wafanyakazi wote.


Hakuna maoni: