Breaking


Ijumaa, 1 Mei 2026

WAZIRI WA NISHATI ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA AFRIKA KUSINI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI


Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini tarehe 29 Aprili 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.


Katika ziara hiyo, Waziri Ndejembi alikutana na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mheshimiwa James Bwana, pamoja na watumishi wa ubalozi huo. Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha sekta ya nishati, kukuza uwekezaji, na kuongeza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini.


Waziri huyo aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, pamoja na ujumbe wa wataalamu kutoka Tanzania waliokuwa wakishiriki mikutano ya kimataifa inayohusiana na miundombinu na nishati.


Ziara hiyo imefanyika sambamba na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Wataalamu ya Umoja wa Afrika kuhusu Uchukuzi na Nishati (STC on Transport and Energy), uliofanyika kuanzia Aprili 27 hadi 29, 2026, pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa Umoja wa Afrika wanaosimamia miundombinu na nishati uliofanyika jijini Johannesburg tarehe 30 Aprili 2026.


Akiwa ubalozini, Mheshimiwa Ndejembi alipata fursa ya kujadiliana na watumishi kuhusu masuala ya maendeleo na fursa zilizopo katika sekta ya nishati. Alisisitiza umuhimu wa kuvutia uwekezaji kutoka Afrika Kusini, hususan katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe, sekta ambayo imeendelea kukua kwa kasi katika taifa hilo.

Aidha, Waziri Ndejembi aliwahimiza wawekezaji kutumia fursa zilizopo nchini Tanzania, akibainisha kuwa mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuboreshwa ili kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi.

Ziara hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendeleza diplomasia ya uchumi kupitia balozi zake, kwa lengo la kukuza biashara, uwekezaji, na ushirikiano wa kimkakati katika sekta mbalimbali.


Hakuna maoni: