MRADI wa Mifumo ya Chakula, Matumizi ya Ardhi na Urejesho wa Mandhari ya Misitu nchini Tanzania (FOLUR), umekutana na viongozi wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Mngeta kwa ajili ya mafunzo maalumu kwa viongozi wa kata na vijiji ambao wako kwenye eneo la mradi.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mratibu wa Mradi Kongani ya Kilombero Halmashauri ya Mlimba, Bw. Joseph Mgana ambaye alisema kuwa kwa sasa wameanza na viongozi wa Kata ya Mngeta ambapo wataenda kwenye kata tano zenye vijiji 23 katika Halmashauri ya Mlimba ambazo zinahusika na Mradi moja kwa moja.
Aidha viongozi wa Kamati ya Maendeleo ya Kata wamefundishwa miongozo mikuu mitatu ya namna bora ya kuepuka migogoro katika utekelezaji wa shughuli za Mradi, mojawapo ikiwa ni Mpango wa Usimamizi wa Mazingira na Jamii (ESMP), ambao unalenga kudhibiti na kupunguza athari za kimazingira na kijamii wakati wa utekelezaji wa Mradi.
Mpango huo unakwenda sambamba na matakwa ya Mwongozo wa Sera na Taratibu Jumuishi za Ulinzi wa Kijamii za Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF).
Aidha, viongozi hao wamefundishwa kuhusu Usimamizi Shirikishi wa Visumbufu, kwa lengo la kulinda afya na usalama wa jamii ili kudhibiti athari zitokanazo na matumizi ya viuatilifu na mbolea.
Katika kuhakikisha usalama wa jamii, mradi pia umeweka utaratibu maalumu wa kupokea na kufanyia kazi malalamiko kutoka kwa jamii au kikundi kuhusiana na shughuli zinazotekelezwa na Mradi.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha jamii inashiriki vema kwenye shughuli za mradi na wanakuwa na nafasi ya kutoa maoni au malalamiko yao wakati wa utekelezaji wa Mradi.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni