Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na ABSA Bank Tanzania wameendesha mafunzo maalum kwa wanawake wajasiriamali yenye lengo la kuwajengea uwezo katika usimamizi wa biashara na fedha.
Washiriki wa mafunzo hayo ni wanachama wa TPSF wanaowakilisha sekta mbalimbali ikiwemo Biashara, Viwanda Vidogo na Vidogo Sana (Small and Micro Industries), Madini, Utalii, Sekta za Ubunifu (Creative Industries) na Wakandarasi. Wanachama hao ni, NABW-TZ, TWCA, TAWOMA, TASSIM, AWOTTA na TANCRAFT.
Mafunzo hayo yalianza kwa wataalamu wa ABSA waliotoa elimu kuhusu usimamizi wa fedha ikijumuisha masuala ya bajeti, akiba na uwekezaji kwa ajili ya kukuza biashara za wajasiriamali.
Baadaye, wataalamu kutoka TRA walitoa elimu kuhusu utii wa kodi (tax compliance) kwa SMEs, wakisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za kodi katika uendeshaji wa biashara.
Kisha Global Alpha Capital walitoa mada kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji na namna wajasiriamali wanavyoweza kunufaika na masoko ya mitaji.
Mwisho, sekta ya bima ilihusika ambapo Jubilee Insurance walieleza kuhusu bima ya maisha, huku Britam Insurance wakifundisha kuhusu bima ya afya kama nguzo muhimu ya usalama wa biashara na familia.
TPSF imesisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia maarifa, mitandao na fursa za kifedha.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni