Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla, ametuma ujumbe wa pongezi na shukrani kwa wafanyakazi wa wakala hiyo katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi 2026.
Katika ujumbe wake, Kihulla ameeleza kuwa siku ya Mei Mosi ni fursa muhimu ya kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika kujenga uchumi imara, hususan kupitia matumizi sahihi ya vipimo vinavyokidhi viwango vya kimataifa.
Amesema anajivunia juhudi, uadilifu na weledi unaooneshwa na wafanyakazi wa WMA katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, ikiwemo uhakiki na ukaguzi wa vipimo pamoja na bidhaa zilizofungashwa.
“Kazi yenu ina mchango mkubwa katika kuimarisha biashara yenye haki, kuongeza imani kwa walaji, na kukuza maendeleo ya taifa letu,” amesema Kihulla.
Aidha, amewapongeza wafanyakazi hao kwa uwezo wao wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia na ukuaji wa sekta mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kujifunza na kuboresha ufanisi kazini.
Kwa upande mwingine, Kihulla amewataka wafanyakazi kuendelea kushirikiana, kudumisha nidhamu ya kazi, na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza tija katika utendaji wao.
Pia ameweka bayana kuwa uongozi wa Wakala wa Vipimo unatambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi wake, na utaendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni