Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeunga mkono kikamilifu jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda na kusimamia mazingira kwa kushiriki zoezi la upandaji miti lililoandaliwa kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, Januari 27.
Katika maadhimisho hayo, Mheshimiwa Rais alipanda mti kama ishara ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira, hatua inayotekeleza kaulimbiu isemayo “Uzalendo ni kutunza mazingira, shiriki kupanda miti.” Kaulimbiu hiyo imelenga kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za vitendo katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia kanda zake 13 zilizopo nchi nzima, NEMC imeshirikiana na wizara mbalimbali, taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia pamoja na kamati za mazingira katika kutekeleza zoezi la upandaji miti katika maeneo tofauti yakiwemo shule, zahanati, masoko na maeneo ya umma.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Bw. Dickson Mjinja, alieleza kuwa upandaji miti ni miongoni mwa njia muhimu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Alisisitiza kuwa miti ina mchango mkubwa katika kuhifadhi ikolojia, kupunguza joto, kuimarisha vyanzo vya maji na kuboresha ustawi wa maisha ya binadamu.
Kwa upande wake, Meneja wa NEMC Kanda ya Ilala, Bi. Abella Muyungi, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kusimamia na kuhifadhi mazingira kwa vitendo, akibainisha kuwa jukumu la uhifadhi wa mazingira ni la kila mmoja bila kujali nafasi au majukumu aliyonayo.
NEMC imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kulinda na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Zoezi la upandaji miti lililofanyika katika Kata ya Ilala, viwanja vya Msikate Tamaa, liliratibiwa na NEMC kwa kushirikiana na Balozi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Grit Godfrey.












Hakuna maoni:
Chapisha Maoni