Breaking


Jumatatu, 9 Machi 2026

MRADI WA TAZA KUWEZESHA MKOA WA RUKWA KUUNGANISHWA NA GRIDI YA TAIFA.


 

Waziri wa Nishati,Deogratous Ndejembi, amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa kuunganisha gridi ya umeme kati ya Tanzania na Zambia (TAZA),unatarajiwa kuleta manufaa makubwa mara utakapokamilika ikiwemo kuimarika kwa upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, pamoja na kuwezesha Mkoa wa Rukwa kuunganishwa rasmi kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa.

Ndejembi ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika kituo cha kupoza umeme cha Iganjo, kilichopo Uyole mkoani Mbeya, ambacho ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo leo tarehe 08 Machi,2026.

Amefafanua kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400, kuanzia Iringa kupitia Kisada, Mbeya na Tunduma hadi Sumbawanga, pamoja na kuunganisha gridi ya umeme ya Tanzania na Zambia katika mpaka wa Nakonde.

Aidha, amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 76, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya umeme na kukuza biashara ya nishati kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini.

Waziri Ndejembi amesema mradi huo utaongeza uwezo wa kusafirisha umeme hadi megawati 1,700, hatua itakayochochea biashara ya umeme kati ya Tanzania na nchi wanachama wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika,utaongeza fursa za ajira kwa wananchi, kuvutia uwekezaji wa viwanda na kukuza shughuli mbalimbali za kiuchumi katika maeneo yanayopitiwa na miundombinu hiyo ya umeme.

Aidha, Waziri huyo ameuagiza uongozi wa TANESCO kuhakikisha mradi huo wa kimkakati unakamilika kwa mafanikio ili kuiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na biashara ya umeme ya kikanda.

Akizungumzia mradi huo, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati Innocent Luoga amesema ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme umefikia asilimia 92.87, huku ujenzi wa vituo vya kupoza umeme ukiwa umefikia asilimia 60.57. 

Kamishna Luoga ameongeza kuwa hadi kukamilika kwa mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 761.8, sawa na takribani shilingi Trilion 2 za Kitanzania.

Hakuna maoni: