Breaking


Ijumaa, 6 Machi 2026

MASAUNI ATOA MAAGIZO MATANO KWA BODI YA NCMC

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ametoa maagizo matano kwa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) mara baada ya kuizindua Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa maagizo hayo ni kuimarisha mifumo ya upimaji, utoaji taarifa na uhakiki wa gesijoto (MRV) ili kuhakikisha taarifa za kaboni nchini zinakuwa sahihi na zinazokubalika kimataifa. Pia ameielekeza bodi hiyo kusimamia kwa uwazi na ufanisi miradi yote ya kaboni, kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo, kuhakikisha mgawanyo wa haki wa manufaa kwa jamii zinazohifadhi rasilimali na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika masoko ya kimataifa ya kaboni chini ya Mkataba wa Paris.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NCMC, Dkt. Albina Chuwa, amesema bodi hiyo itahakikisha inaimarisha ushirikiano wa wadau ili kusimamia vizuri rasilimali za kaboni na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Amesema Uzinduzi wa Bodi unakuja katika kipindi muhimu ambacho sekta ya biashara ya kaboni inaendelea kukua kwa kasi duniani na hapa nchini, NCMC ina jukumu muhimu la kuhakikisha kuwa rasilimali za kaboni za nchi yetu zinasimamiwa kwa uwazi, weledi na kwa kuzingatia mifumo na viwango vinavyokubalika kimataifa.


Wajumbe wanaounda Bodi hiyo ni Bw. Khamis Hamza Khamis, Bi. Amne Sued Kagasheki, Bi. Farhat Mabrouk, Dkt. Ladislaus Kyaruzi, Bw. Rishad Bade pamoja na Dkt.Philipina Fenest Shayo

Hakuna maoni: