Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa Machi 19, 2026, ikionesha kuwa maeneo mengi nchini yanatarajiwa kuwa na hali ya mawingu, mvua pamoja na ngurumo za radi katika maeneo machache.
Kwa mujibu wa utabiri huo, mikoa ya pwani ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba itashuhudia vipindi vya mvua vinavyoweza kuambatana na jua kwa muda mfupi, huku maeneo ya kaskazini na nyanda za juu yakitarajiwa kuwa na hali ya baridi kiasi na mvua za hapa na pale.
Aidha, TMA imetoa tahadhari ya uwepo wa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya mikoa ikiwemo Kigoma, Katavi, Rukwa, Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga, Dar es Salaam na Pwani pamoja na visiwa vya Zanzibar.
Wananchi katika maeneo hayo wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza, ikiwemo mafuriko ya muda mfupi. Kwa upande wa hali ya bahari, mawimbi yanatarajiwa kuwa madogo huku upepo ukivuma kutoka kusini mashariki kwa kasi ya takribani kilomita 20 kwa saa katika ukanda wote wa pwani.
Kwa upande wa viwango vya joto, miji mbalimbali inatarajiwa kuwa na hali ya joto la wastani, ambapo Dar es Salaam itakuwa na nyuzi joto kati ya 24°C hadi 30°C, Arusha 16°C hadi 26°C, huku Tanga na Zanzibar zikifikia hadi 32°C.
Miji ya nyanda za juu kusini kama Njombe na Mbeya inatarajiwa kuwa na hali ya baridi zaidi ikilinganishwa na maeneo ya pwani.
TMA imeeleza kuwa mabadiliko madogo ya hali ya hewa yanatarajiwa kuendelea hadi siku ya Jumamosi, hivyo wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni