Breaking


Alhamisi, 14 Mei 2026

AFUNGWA JELA BAADA YA KUIBA MUZIKI WA BEYONCE AMBAO HAUJATOLEWA

Mwanamume mmoja nchini Marekani amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kuhusishwa na wizi wa kifaa cha kuhifadhi taarifa (hard drive) kilichokuwa na muziki wa msanii maarufu Beyoncé ambao haukuwa umetolewa rasmi kwa umma.


Mtuhumiwa huyo, Kelvin Evans mwenye umri wa miaka 41, alikiri makosa mbalimbali ikiwemo kuvunja gari na kuiba mali katika tukio lililotokea mwaka 2025 mjini Atlanta, Georgia. Mahakama pia imemuhukumu miaka mitatu ya kufuatiliwa tabia baada ya kumaliza kifungo chake gerezani.


Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, Evans alivunja gari aina ya Jeep Wagoneer lililokuwa limekodishwa na mmoja wa wacheza densi pamoja na mpiga ngoma wa Beyoncé wakati ziara ya Cowboy Carter ikiendelea jijini humo mnamo Julai 8, 2025. Waathiriwa waliporudi walikuta dirisha la nyuma la gari limevunjwa huku mizigo na vifaa vyao vikiwa vimeibwa.


Inadaiwa hard drive hiyo ilikuwa na nyimbo ambazo bado hazijatolewa pamoja na taarifa nyingine muhimu zinazohusiana na kazi za msanii huyo. Hata hivyo, wachunguzi wamesema hadi sasa vifaa hivyo bado havijapatikana.


Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Fulton County imethibitisha kuwa Evans alifikia makubaliano ya kukiri mashtaka kabla ya kesi kuanza rasmi. Kama sehemu ya hukumu yake, ameamriwa pia kutokaribia waathiriwa wala eneo la maegesho ambako tukio hilo lilitokea.


Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa kuhusu usalama wa kazi za wasanii na umuhimu wa kulinda hakimiliki dhidi ya wizi wa kidijitali katika tasnia ya muziki duniani.


Hakuna maoni: